Karibuni! Katika kurasa zinazofuata, tunawapatia taarifa na sifa bainifu zinazowatofautisha mamalia wa Tanzania. Taarifa na sifa hizo zitakuwezesha kutofautisha na kutambua fuu au ngozi za karibu mamalia wote wanaopatikana Tanzania. Ingawa kurasa hizi za webu zilitayarishwa kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta ya maliasili, tunategemea kwamba zitawavutia pia na kuwa na manufaa kwa washabiki wote wa mamalia.

Tumetoa aina mbili za taarifa na sifa bainifu za mamalia. Aina ya kwanza ya taarifa zinamtofautisha mamalia mzima (siyo mtoto) kwa kuangalia ngozi tu (na mara nyingine, baadhi ya sifa bainifu zilizopo mdomoni). Aina ya pili zinamtofautisha mamalia kutokana na sifa bainifu za fuu lake tu. Taarifa na sifa hizi haziwezi kutoa majibu sahihi iwapo zitatumika kutofautisha mamalia watoto. Aina zote mbili zimetayarishwa ili zitumike kwa wakati mmoja ukiwa umeshika kielelezo (ngozi au fuu lisilo na nyama wala ngozi) mkononi na ukiangalia Webu (World Wide Web), darubini na kalipa (inapowezekana) au lenzi ya mkono na rula.

Mamalia waliomo katika makala hii ni wale wanaopatikana Tanzania, kufuatana na kitabu chenye kichwa cha Check-list of the Mammals of East Africa, kilichochapishwa na East Africa Natural History Society mwaka 1994. Ingawa inawezekana kwamba baadhi ya mamalia hawakuorodheshwa katika Check-list of the Mammals of East Africa na kwa hiyo hawamo kwenye makala yetu hii, tumejitahidi kuorodhesha karibu mamalia wote wa Tanzania. Taarifa na sifa bainifu hizi zimetayarishwa kwa namna ambayo inakuwa rahisi kuongeza mamalia wengine, kila aina nyingine ya mamalia inapogunduliwa Tanzania. Kwa sasa, taarifa hizi zinakomea kwenye kiwango cha jenasi (genus). Baadaye, tunatarajia kutoa taarifa za spishi (species) za kila jenasi.


Wakati wa kutayarisha makala hii, tumetumia kumbukumbu mbalimbali na nzuri sana ambazo zimeorodheshwa katika Marejeo, kwenye sehemu ya Shukrani. Kumbukumbu hizi zinatoa taarifa nyingi za ziada juu ya mamalia wa Tanzania.

Kazi ya kutayarisha taarifa na sifa bainifu inaendelea na inahitaji mchango wa watumiaji wa taarifa hizi. Kwa hivyo tungependa kupokea maoni yenu kuhusu makala hii. Tafadhali tuma maoni au maswali yako kwa Bill Stanley kwa kutumia anwani ya e-mail ifuatayo: tanzaniakey@fieldmuseum.org

Tafadhali bonyeza kwenye sehemu zinazohusika za skrini ili upate maelekezo juu ya utumiaji wa taarifa hizi. Kabla ya kutumia taarifa na sifa bainifu zetu, tunawashauri wote wanaotumia taarifa hizi kwa mara ya kwanza wasome kwanza sehemu ya Maelekezo.











Kiswahili Home | Maelekezo | Fuu | Ngozi | Safu Za Milima Ya Mashariki | Zoology | Field Museum Home | Shukrani Na Marejo | Tanzanian Mammal Key (English Version)

© 2007 The Field Museum, All Rights Reserved
1400 S. Lake Shore Dr., Chicago, IL 60605-2496
312.922.9410